Comment

Darasa Huru

Darasa Huru

Limitless Potential

We provide the tools. You make the grade.

Topic

Uhakiki Wa Kazi Za Fasihi Andishi

Estimated reading: 96 minutes 544 views

Summary: Fasihi andishi ni tawi la fasihi linalotumia sanaa ya maneno kufikisha ujumbe kwa hadhira kwa njia ya maandishi. Zipo aina nyingi za fasihi andishi, miongoni mwa hizo ni pamoja na hadithi fupi, riwaya, tamthiliya na mashairi.

UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI

Maana ya Uhakiki

Uhakiki ni kitendo cha kutathmini, kueleza, kuainisha, na kutoa maoni juu ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalum. Hii ina maana kwamba uhakiki wa kazi za fasihi hautoki katika ombwe; kuna kanuni na taratibu mbalimbali zinazoongoza kufanya uhakiki. Hii ndio sababu kuna nadharia kadha wa kadha za uhakiki wa kazi za kifasihi. Kwa lugha rahisi, uhakiki ni uchambuzi wa kina wa kazi za fasihi kama vile riwaya, tamthiliya, na mashairi kwa lengo la kufafanua vipengele vya fani na maudhui.

Misingi ya Uhakiki

Kwa ujumla, mhakiki wa kazi za fasihi anapofanya uhakiki wa kazi za kifasihi huwa analenga vipengele viwili: fani na maudhui ya kazi hiyo, na wakati mwingine vyote viwili. Kupitia vipengele hivi, mhakiki huchambua vitu vingi kama vile ujumbe, falsafa, matumizi ya lugha, dhamira, na mandhari.

Kuhakiki Fani

Katika utunzi wa kazi za kifasihi, fani hutumika kama nyezo ya kuwasilisha mawazo ya mwandishi kwa njia ya kisanaa zaidi. Fani ni mbinu anayoitumia mwandishi ili kufikisha ujumbe kwa watu aliowakusudia. Vipengele vya fani ni pamoja na wahusika, mandhari, lugha, muundo, na mtindo.

Mtindo

Mtindo ni mbinu ya kipekee kifani na kimaudhui zinazotofautisha msanii mmoja na mwingine. Kwa mfano, namna msanii anavyotumia lugha, anavyoteua msamiati, na namna anavyosimulia hadithi yake. Mfano mzuri ni riwaya ya “Barua Ndefu Kama Hii” iliyoandikwa na Mariama Ba, ambapo ametumia mtindo wa barua ya kirafiki kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Muundo

Muundo ni mpangilio wa kiufundi anaoutumia mwandishi katika kupangilia kazi yake. Huu ni mpangilio na mtiririko wa kazi ya fasihi, kwa upande wa visa na matukio. Kuna aina mbili za kupangilia matukio:

  • Msago: Namna ya moja kwa moja ya kusimulia matukio, kuanzia tukio la kwanza hadi la mwisho kwa namna yalivyotukia.
  • Urejeshi: Usimuliaji wa kurukaruka hatua, ambapo msimuliaji anaweza kuanzia katikati, akaja mwisho na kumalizia na mwanzo.

Wahusika

Wahusika ni watu au viumbe ambavyo mwandishi wa fasihi huwatumia ili kufanikisha ujumbe kwa jamii husika. Wahusika hugawanywa katika makundi mawili: wahusika wakuu na wahusika wadogo. Wahusika hawa huweza kugawanyika katika makundi yafuatayo:

  • Mhusika mviringo: Mhusika ambaye anabadilika kitabia na kimawazo kulingana na hali halisi ya maisha.
  • Mhusika bapa: Mhusika ambaye habadiliki kulingana na hali halisi ya maisha.
  • Mhusika shinda: Yuko katikati ya mhusika bapa na mviringo. Huongozwa na matendo ya hao wahusika wawili.

Mandhari

Mandhari ni sehemu ambayo matukio ya hadithi au masimulizi hutokea. Mandhari huweza kuwa halisi kama vile baharini, njiani, msituni, kijijini, au ya kufikirika kama vile kuzimu, mbinguni, peponi n.k.

Lugha

Lugha ndio nyenzo kubwa ya msanii katika kazi za fasihi. Vipengele vya lugha ni tamathali za semi pamoja na semi. Fani za lugha ni pamoja na:

  • Tanakali za Sauti: Maneno yanayoiga sauti au hali fulani.
  • Tashbiha: Linalinganisha vitu au hali mbili tofauti kwa kutumia maneno kama ‘kama’, ‘mithili ya’, ‘sawa na’, ‘ja’. Mfano, “Mwembamba kama sindano”.
  • Tashihisi: Mbinu ya kupatia kitu kisicho hai sifa za kiumbe mwenye uhai. Mfano, “Sungura aliposhindwa, akasema sizitaki hizi mbichi”.
  • Takriri: Kurudiarudia neno moja au kifungu cha maneno ili kusisitiza ujumbe fulani. Mfano, “alikimbia, alikimbia, alikimbia hadi akashika nafasi ya kwanza”.
  • Ukinzani: Mbinu ya kusisitiza ujumbe kwa kuambatanisha maneno ya kinyume au yanayokinzana.
  • Sitiari: Linalinganisha vitu viwili moja kwa moja kwa kutumia kiungo ‘ni’ ama ‘kuwa’. Mfano; “Maisha ni mlima, Juma ni mwamba”.
  • Taswira: Matumizi ya lugha/maneno yanayojenga picha ya hali au jambo fulani kwa msomaji.
  • Taashira: Matumizi ya lugha ya ishara kuwakilisha ujumbe fulani.
  • Jazanda: Kulilinganisha vitu viwili moja kwa moja bila kutumia viunganishi.
  • Majazi: Tabia za wahusika zinapoambatana na majina yao halisi.
  • Lakabu: Mhusika kupewa/kubandikwa jina linalooana na tabia/sifa zake.
  • Chuku: Kutumia maneno yaliyotiliwa chumvi ili kusisitiza ujumbe fulani au kusifia kitu.

Semi

Semi ni fungu la maneno linapotumika kutoa maana nyingine, badala ya ile ya maneno yaliyotumika. Semi hutumika kuficha ukali wa maneno au kupamba lugha. Kuna aina mbili za semi:

  • Nahau: Usemi unaotumia maneno ya kawaida kwa lengo la kufikisha maana iliyotofauti na maana ya kawaida ya maneno hayo. Nahau huwa na vitenzi.
  • Misemo: Semi fupifupi ambazo hutumiwa mara kwa mara kwa lengo la kuleta maana maalumu. Misemo haina vitenzi.

Maswali ya Balagha

Maswali ya balagha ni maswali yanayoulizwa na msimulizi au mhusika ambayo hayahitaji jibu.

Uzungumzi Nafsiya

Mhusika hujizungumzia, ama kwa kuongea au kuwaza, bila kukusudia kusikika na yeyote.

Ritifaa

Mbinu ya kuzungumza na mtu aliyekufa (au asiyekuwepo) kana kwamba yuko pamoja nawe.

Kuchanganya Ndimi

Kuweka maneno yasiyo ya Kiswahili katika sentensi ya Kiswahili. Mfano, “alisimama kwanza kwa muda, before he went aliniambia nisimwambie mtu yeyote yule, you know!”

Kuhamisha Ndimi

Ni kuingiza sentensi ya lugha nyingine katika kifungu cha lugha ya Kiswahili. Kinyume na Kuchanganya Ndimi, sentensi kamilifu ya lugha nyingine hutumika miongoni mwa sentensi za Kiswahili sanifu.

Mathali

Methali ni misemo ya hekima yenye maana iliyofumbwa. Mhusika au mwandishi wa fasihi anaweza kutumia methali kupitisha ujumbe.

Mbinu Nyingine za Kisanaa

Kinaya

Kinaya ni mambo katika sanaa kuwa kinyume na matarajio ya hadhira.

Kejeli

Kejeli ni mbinu ya sanaa inayotumia maneno kudharau au kukemea kitendo au mtu fulani.

Taharuki

Taharuki ni mbinu ya kusimulia au kuandika riwaya/hadithi kwa kufanya hadhira na/au wahusika wajawe na hamu ya kutaka kujua kitakachotokea baadaye; hamu ya kutaka kuendelea kusoma/kusikiliza.

Sadfa

Sadfa ni kugongana kwa vitendo viwili vinavyohusiana kana kwamba vilikuwa vimepangwa, japo havikuwa vimepangiwa.

Kisengere Nyuma

Mwandishi ‘hurudi nyuma’ na kuanza kusimulia kisa kilichokuwa kimetendeka kabla ya alichokuwa akisimulia.

Kisengere Mbele

Mwandishi anapobadilisha wakati na kusimulia mambo yatakavyokuwa siku za usoni au kutumia lugha isiyo moja kwa moja kutabiri yatakayojiri.

Kuhakiki Maudhui

Maudhui:
Maudhui katika kazi ya fasihi ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo. Maudhui hujumuisha mawazo na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi akatunga kazi fulani ya kifasihi. Vipengele vya maudhui ni pamoja na dhamira, migogoro, falsafa, ujumbe, na msimamo.

Dhamira:
Dhamira ni wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Dhamira ni sehemu ya maudhui na aghalabu dhamira kuu ndio hujenga kiini cha kazi ya fasihi. Dhamira zimegawanyika katika makundi mawili: dhamira kuu na dhamira ndogondogo.

Migogoro:
Migogoro ni mivutano na misuguano mbalimbali katika kazi za fasihi. Migogoro inaweza kuwa kati ya wahusika, familia zao, matabaka yao, au hata katika nyadhifa mbalimbali. Migogoro yaweza kuwa ya kiuchumi, kijamii, nafsi, na kisiasa, na hujitokeza katika mitazamo tofauti kulingana na mtiririko wa visa na matukio yanavyopangwa na mwandishi.

Ujumbe:
Mwandishi anapoandika kazi yake huwa na ujumbe ambao hutaka uifikie jamii aliyoikusudia. Ujumbe katika kazi fasihi ni mafunzo mbalimbali ambayo hupatikana baada ya kusoma kazi ya fasihi. Katika kazi ya fasihi, dhamira kuu hubeba ujumbe wa msingi na dhamira ndogondogo hubeba ujumbe ambao husaidia kuujenga au kuupa uzito zaidi ujumbe wa msingi.

Msimamo:
Katika kazi ya fasihi, mawazo, mafunzo na falsafa ya msanii hubainisha msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Msimamo ni ile hali ya mwandishi kuamua kufuata na kushikilia jambo fulani. Jambo hili huweza kukataliwa na wengi lakini mwandishi analishikilia tu. Msimamo ndio huweza kuwatofautisha wasanii wawili au zaidi wanaoandika kuhusu mazingira yanayofanana.

Falsafa:
Falsafa ni mawazo ya busara yenye kutawaliwa na misingi mahususi juu ya asili na maana ya ulimwengu na maisha ya mwanadamu. Ni msimamo wa msanii katika maisha juu ya utatuzi wa matatizo katika jamii. Falsafa ya mwandishi inaweza kujulikana kwa kusoma kazi zake zaidi ya moja.

Mtazamo:
Mtazamo ni hisia au uelewa wa mwandishi juu ya jambo fulani. Kwa mfano, mwandishi anaweza kutazama jambo fulani kwa mtazamo wa kidini, kisiasa, au kisayansi.

Mafunzo:
Mafunzo ni mawazo ya kuelimisha yanayopatikana katika dhamira mbalimbali za kazi ya fasihi.

Kufaulu na Kutofaulu kwa Mwandishi

Kufaulu au kutofaulu kwa mwandishi kunategemea jinsi alivyoweka uwiano mzuri kati ya fani na maudhui kwa namna ambayo inaleta uhalisia. Mfano, msanii akiwa na mhusika Mkongo lakini anazungumza Kiswahili kilichojaa misemo na nahau ya Pwani (Tanzania), itakuwa vigumu kusema amefaulu kwani hakuna uwiano mzuri kati ya mhusika mwenyewe na lugha anayoitumia. Kiswahili cha Kongo ni tofauti kabisa na Kiswahili kinachozungumzwa na watu wa Pwani.

Soma Uhakiki wa kazi za Fasihi Andishi ukurasa unaofuata

Leave a Comment

Share this Doc

Uhakiki Wa Kazi Za Fasihi Andishi

Or copy link

CONTENTS

Agricultural Development

What is Agriculture? Agriculture refers to a fundamental human activity, which i...

Population and Development

POPULATION STUDIES Is the general activities carried out for the purpose of acqu...

Study of Soil

CONCEPT OF SOIL AND SOIL PROFILE Soil appears very complex and thus differe...

Water Masses

GROUND WATER WATER CYCLE Rain falls on the earth surface in filtrates (soaks int...

Topic

The Dynamic-Earth And Consequence

THEORIES THEORY OF ISOSTASY Denudation has been going on the continents where to...

Position Behaviours And Structure Of The Earth

GLOBE Is the model of the earth Earth Is ball of rock partly covered by wat...

Photograph interpretation

Photograph are the true image pictures showing truly appearance of the earth’s...

Maps and map interpretation

What is a map? Map is a scaled conventional representation of the whole or any o...

Simple survey and mapping

INTRODUCTION TO SURVEYING Surveying is an art or a science of measuring and reco...

Field research techniques

Definitions of Research – Research is the systematic investigation into a...

Application of statistics in geography

STATISTICS Statistics is a branch that deals with every aspect of the data. Stat...

Chat Icon Close Icon

Subscribe

×
Cancel